Alhamisi 5 Juni 2025 - 17:20
Ulimwengu wa Kiislamu unahitaji kutumia mafundisho ya Hija ili kukomesha maafa huko Ghaza

Hawza/ Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu katika ujumbe wake kwa Mahujaji wa Nyumba ya Mwenyezi Mungu amesisitiza umuhimu wa kutumia mafundisho ya Hija na Ulimwengu wa Kiislamu kwa ajili ya kukomesha maafa huko Ghaza.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, ujumbe wa Hadhrat Ayatollah Khamenei – Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu – ambao ulisomwa asubuhi ya leo (Alhamisi) na Hujjatul-Islam wal-Muslimin Nawwab (mwakilishi wa Waliyy Faqih katika masuala ya Hija na ziara na kiongozi wa mahujaji wa Iran) katika jangwa la Arafah, unasomeka kama ifuatavyo:

بسم‌الله الرّحمن الرّحیم

.والحمدلله ربّ العالمین و الصّلاة و السّلام علی خیر خلق‌الله محمّدٍ المصطفی وآله الطّیّبین وصحبه المنتجبین ومن تبعهم باحسان الی یوم‌الدّین

Kwa jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa Rehema Mwenye Kurehemu
Na himidi zote ni za Mwenyezi Mungu Mola Mlezi wa walimwengu, na rehema na amani zimshukie mbora wa viumbe wa Mwenyezi Mungu, Muhammad al-Mustafa, na watu wa nyumba yake watoharifu, na maswahaba wake wateule, na wale waliowafuata kwa wema hadi Siku ya Malipo.

Hija ni tamanio la waumini, sikukuu ya walio na shauku, na riziki ya kiroho ya waliobarikiwa; na iwapo itatekelezwa kwa maarifa ya undani wa siri zake, basi huwa tiba ya maumivu makuu katika Umma wa Kiislamu, hata kwa wanadamu wote.

Safari ya Hija si kama safari nyingine zinazofanywa kwa ajili ya biashara au utalii au malengo mengine mbalimbali ambazo huenda wakati mwingine ndani yake kukafanyika ibada au kitendo chema; bali safari ya Hija ni mazoezi ya kuhama kutoka maisha ya kawaida kuelekea maisha bora. Maisha bora ni yale ya tauhidi, maisha ambayo katika hayo kuna: Tawafu ya kudumu kuzunguka mhimili wa haki, Sa‘y ya kudumu baina ya vilele vigumu, Kumrushia mawe shetani muovu kwa kudumu, Kusimama katika hali ya dhikri na dua ya unyenyekevu, Kuwalisha masikini waliodhoofika na wasafiri, Kuuona ubinadamu kuwa mmoja bila ya kubagua rangi, kabila, lugha wala jiografia, Kuwa tayari kila wakati kuhudumia, kumkimbilia Mwenyezi Mungu, na kuinua bendera ya kutetea haki – mambo haya yote ni sehemu kuu na ya kudumu.

Ibada ya Hija imekusanya ndani yake mifano ya maisha haya ya kiishara, na inamtambulisha na kumwalika hujaji kwenye maisha haya.

Wito huu unapaswa kusikilizwa; moyo, na macho ya dhahiri na ya batini yafunguliwe; ni lazima kujifunza na kuthibitisha azma ya kutumia mafundisho haya. Kila mmoja, kwa kadiri ya uwezo wake, anaweza kuchukua hatua katika njia hii; na wanazuoni, watu wa fikra, wanasiasa na wenye nafasi za kijamii, wanawajibika zaidi kuliko wengine.

Leo hii, ulimwengu wa Kiislamu unayahitaji mafundisho haya zaidi kuliko wakati mwingine wowote. Huu ni msimu wa pili wa Hija unaofanyika wakati ambapo maafa ya Ghaza na Asia ya Magharibi yanaendelea. Kundi la Kizayuni la kihalifu linalotawala Palestina, kwa ukatili wa kushangaza na uovu wa kupindukia, limelifikisha janga la Ghaza katika hatua ya kustaajabisha. Sasa hivi watoto wa Palestina hawauawi tena kwa mabomu na risasi tu, bali hata kwa kiu na njaa; idadi ya familia zinazopoteza wapendwa wao, vijana, baba na mama inaongezeka kila siku. Ni nani anayepaswa kusimama dhidi ya janga hili la kibinadamu?

Bila shaka, serikali za Kiislamu ndizo walengwa wa kwanza wa jukumu hili, na mataifa yanapaswa kudai watawala wao kutekeleza jukumu hilo. Huenda serikali za Kiislamu zikawa na tofauti za kisiasa katika masuala mbalimbali, lakini hili haliwezi na halipaswi kuzuia kuafikiana na kushirikiana kuhusu suala hili zito la Ghaza na katika kutetea kundi lililoonewa zaidi katika dunia ya leo.

Serikali za Kiislamu zinapaswa kuzifunga njia zote za kuusaidia utawala wa Kizayuni, na kuuzuia mkono wake wa kihalifu kuendeleza uovu huko Ghaza.

Marekani ni mshirika wa dhati katika jinai zinazofanywa na utawala wa Kizayuni; washirika wa Marekani katika eneo hili na maeneo mengine ya Kiislamu wanapaswa kulisikiliza neno la Qur'an kuhusu kutetea wanyonge, na kulazimisha serikali ya kibeberu ya Marekani kuacha tabia hii dhalimu. Ibada ya "barā’a" katika Hija ni hatua katika njia hii.

Muqawama wa kushangaza wa watu wa Ghaza umeliweka suala la Palestina katika nafasi ya juu zaidi katika fikra za ulimwengu wa Kiislamu na wote wanaopigania haki duniani; fursa hii inapaswa kutumika kwa haraka, na lazima kuikimbilia kuisaidia jamii hii iliyodhulumiwa.

Licha ya juhudi za mabeberu na wafuasi wa utawala wa Kizayuni za kulifanya suala la Palestina lisahaulike, asili ovu ya viongozi wa utawala huu na siasa zao za kijinga zimezua hali ambayo leo hii jina la Palestina linang'aa kuliko wakati mwingine wowote, na chuki ya watu kwa Wazayuni na wafuasi wao ni kubwa kuliko wakati mwingine wowote; na hii ni fursa muhimu sana kwa ulimwengu wa Kiislamu.

Wasemaji na watu wenye nafasi katika jamii wanapaswa kuyaamsha mataifa mbalimbali na kuwafanya waelewe, na kupanua madai kuhusu Palestina. Nanyi mahujaji mliojaliwa riziki hii ya kimaanawi, msipuuze fursa ya dua na kumuomba Mwenyezi Mungu katika ibada za Hija, na muombe ushindi dhidi ya madhalimu wa Kizayuni na wafuasi wao kutoka kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu.

Sala na salamu za Mwenyezi Mungu zimshukie Mtume mtukufu wa Uislamu na watu wa nyumba yake waliotakasika, na salamu na amani zimshukie Bwana wetu Mahdi Bāqiyyatu-llāh (aj).

والسّلام علیکم و رحمة‌الله و برکاته

Sayyid Ali Khamenei

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha